Mage wa tanga anasema; “Niliolewa miaka sita iliyopita, mume wangu ni mfanyakazi mwenzangu katika Halimashauri moja hapa nchini mimi nilikua katibu muhtasi. Baada ya kuoana mume wangu alitaka niache kazi kwakuwa mshahara wangu ulikuwa mdogo na ulikuwa hauchangii chochote ukilinganisha na mshahara wake.
Mshahara wake ulikuwa ni zaidi ya mara kumi ya mshahara wangu, kwani yeye ni mkuu wa idara hivyo ana mshahara mkubwa na marupurupu yake pia yalikuwa ni mengi. Kusema kweli hata mimi mwenyewe sikutaka kuendelea tena kufanya kazi ile, lakini pia sikutaka kukaa tu nyumbani bila kitu cha kufanya, tulikubaliana anifungulie biashara ili na mimi nisikae tu.
Miezi miwili baada tu ya kuacha kazi nilipata ujauzito hivyo suala la biashara likasimama kwa muda, kwakuwa sikuwa na shida yoyote ya kifedha sikuwa na haraka ya kufanya biashara, kila nilichokuwa nikikihitaji nilikipata. Nilipojifungua nilitaka kumlea mwanangu kwanza kabla ya kuanza kujishughulisha.
Alipofikisha miaka miwili ndipo wazo la biashara liliponijia tena, lakini kwa bahati mbaya kabla sijaanza kufanya chochote mama yangu alianza kuumwa hivyo nikalazimika kukaa naye kumuuguza. Miezi sita baadaye mama yangu alipona na kurejea kijijini, mimi na mume wangu tuliona ndiyo wakati muafaka wa mimi kuanza kufanya biashara.
Wakati bado nawaza biashara gani ya kufanya niligundua kua nina ujauzito wa mtoto wangu wa pili. Hapo tena suala la biashara likasimama nikisubiri nijifungue na mwanangu akuekue. Nilifanikiwa kujifungua salama mtoto wa kike, nikiwa hata bado sijamaliza arubaini kwa bahati mbaya mume wangu alipata ajali ya gari na kufariki.
Maisha yangu nikama yalifika mwisho kwani yeye ndiye alikuwa ni kila kitu katika maisha yangu. Bado nilikuwa na watoto wadogo wa kuwalea, kazi nilikuwa nimekwisha acha, wakati huo bado tulikuwa tukiishi nyumba ya kupanga na mume wangu alishanunua kiwanja na kaunza ujenzi ambao ndio kwanza ulikuwa upo hatua ya lenta.
Yeye ndiyo alikuwa akitegemewa na kila mtu, kuanzia ndugu zake pamoja na ndugu zangu. Alikuwa akiwasomesha wadogo zangu pamoja na wadogo zake, alikuwa akihudumia familia zote mbili, kusema kweli hatukuwekeza sana lakini ni kwasababu ya majukumu ambayo alikuwa nayo.
Maisha yalibadilika, hata akiba tuliyokuwa nayo na mafao tuliyolipwa havikutosha kutatua matatizo yetu. Migogoro ya kugombea mali ilizuka na nilijikuta nanyang’anywa kila kitu na kubaki na watoto wangu tu ambao bado walikuwa wadogo. Ndugu ambao awali tulikuwa tukiishi nao vizuri na mume wangu alikuwa akiwasaidia sasa hata simu zangu hawapokei.
Kusema kweli nimechanganyikiwa kaka na sijui nifanyeje, kila kitu katika maisha yangu kimegeuka juu chini hata kodi ya nyumba sasa ni shida. Maisha yamekuwa magumu sijui hata nifanyeje, najaribu kutafuta kazi lakini sipati imekuwa vigumu sana kupata kazi, sijui hata wanangu watasomaje natamani kufanya biashara lakini sina mtaji. Naomba unisaidie Kaka hata kwa mawazo tu niweze kujikwamua” Anamalizia Mage.
KABLA HUJAACHA KAZI SOMA KISA CHA KWANZA MAGE WA TANGA
Reviewed by Love Psychologist
on
February 28, 2019
Rating:

No comments: