Sponsor

banner image

recent posts

SIMULIZI FUPI: HUYU NDIYE MAMA YANGU MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA

SIMULIZI FUPI: HUYU NDIYE MAMA YANGU MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA


MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA
Kwa: wanawake wote!!
TETESI zilizokuwa zimezagaa mtaani zilinitatanisha sana, nilijua kuwa kila nilipokuwa napita basi watu walinyoosheana vidole na kusema lolote ambalo waliweza kusema.
Ni kweli sikujua rasmi ni maneno gani walikuwa wanasema lakini hayakuwa mazuri.
Ningeweza vipi sasa kuwazuia watu kusema wakati walikuwa wamepewa vinywa ili waweze kusema. Niliyaishi maisha yangu bila kujishughulisha na maneno yao, ilikuwa ngumu lakini niliweza.
Nilijua kilichokuwa kinawachanganya zaidi ni maisha yangu duni, kulalia mkeka pamoja na kuwa na sufuria mbili ndogo.
Nilitabasamu na kujiuliza ikiwa wanapenda niwe na maisha bora basi na waninunulie vitu wanavyotaka niwe navyo na hapo watakuwa na haki ya kusema lolote.
Nilizisikia tetesi eti wananiita mimi mshirikina, wengine wakazusha eti mimi ni jambazi na nimejenga majumba mengi ya kifahari.
Nikatabasamu na kumega tonge la ugali nikalichovya katika mlenda wangu nikalimeza likadondoka tumboni kunipa shibe mimi siku ziendelee.
Sikujua wenzangu kuwa maisha yasiyowahusu yalikuwa yanawanyima amani kabisa na ikafika siku ya siku ile naamka tu nakutana na lundo la watu mlangoni kwangu.
Nikajiuliza je litakuwa ni tatizo la kodi au? Lakini kodi yote nilikuwa nimelipa, kama ni usafi nilikuwa nafanya kila inapofika zamu yangu, sasa ni kitu gani kimewaleta pale katika mlango wangu.
Nikatoka nje na hapo nikakutana na mikono iliyobeba mawe, mapanga na marungu!!
Moyo wangu ukapiga kwa nguvu sana, nikajiuliza ni kitu gani tena hiki kinanitokea mimi. Nikiwa bado sijapata jibu kijana mmoja mbabe wa umbo akawatuliza wenzake kisha akazungumza.
“Akilimali unashutumiwa kwa wizi wa kuvunja na kuiba kwenye duka la mzee Yahaya, hatupo hapa kwa ajili ya shari bali kuzirudisha pesa zote ulizochukua katika meza iliyopo pale…” kabla hajamalizia mama mmoja mfupi mweusi akadakia, “Unamweleza nini sasa wakati anajua ni meza ipi inayozungumziwa mbona unambembeleza….”
Yule kijana akaendelea!!
“Tupatie hizo pesa nasi tutakupeleka polisi tu lakini kama hautoi pesa hata polisi haufiki tutakuua hapahapa huu mtaa haujawahi kuwa na wezi kabla haujahamia hapa Akilimali. Ni kitu gani hiki unatuletea katika mtaa wetu……” alizungumza kwa jazba. Kisha mwanamke mwingine naye akadakia.
“Hata mtu hajulikani dada, baba, wala kaka yake mtu gani huyu asiyekuwa hata na mama wa kumtembelea walau tumjue….”
Alipomaliza kuzungumza palikuwa kimya. Nilijua kuwa jambo lililokuwa mbele yangu halikuwa dogo hivyo nilitakiwa kuwa mtulivu na mwenye busara haswa!!
Nikajikohoza wakatulia kunisikiliza. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuzungumza mbele ya kundi la watu kama vile.
“Niliisubiri hii siku kwa hamu ya kuzungumza nanyi katika umoja huu, nisingeweza kumfuata kila mmoja na kuzungumza naye japokuwa niliyasikia maneno yenu sana tu wanaume kwa wanawake wakubwa kwa wadogo. Imekuwa heri imekuwa siku hii, kabla sijaanza kuzungumza nawahakikishia kuwa sina pesa ya mtu na nikimaliza kuzungumza natoa ruhusa kwa yeyote anayeweza kuua na aniue mimi… sina chochote cha kusema ni urithi, mkeka wangu huu atakayeona yafaa basi ataupeleka katika kituo cha watoto yatima wanahitaji sana kwa ajili ya kujihifadhi usiku, na sufuria zangu hizi ziende hukohuko. Ewe mwanamke uliyeupaza mdomo wako eti wataka kumjua mama yangu napenda nikuelezee juu ya mama yangu wewe na wenzako wote wamsikie na kumjua.
Mama yangu ni kahaba muda kama huu amelala hoi kitandani kutokana na suluba ambazo nyinyi wanaume mmepa usiku wa manane, mlioutumia mwili wake na kuacha kumlipa, mama yangu yupo jalalani sasa amechanganyikiwa kutokana na ugumu wa maisha na baadaye wajinga wajinga kati yenu waka,mbaka akakumbwa na kichaa cha mimba yupo majalalani anakula makombo yenu mama yangu yu hai anaishi, anaishi katika nyumba zenu mama yangu ni mtu mbaya sana mama yangu ni yule mama wa kambo ambaye haoni kama ni haki yule mtoto mdogo pale nyumani akitabasamu walau kwa sasa moja tu, anamuonea na kumkosea haki zake pasi na sababu mama yangu ni mbaya kiasi hicho na sidhani kama mngetamani kumuona, yupo mama yangu na anaishi na muda huu ninaozungumza na mimi yupo hospitali akitoa mimba ya ambaye angekuja kuwa mdogo wangu, simpendi mama yangu na kama hamuamini basi muende hospitali sasa mtamkuta akiwa na mwanaume anayejiita daktari wakishirikiana kumuua mdogo wangu, wakati mwingine simlaumu mama yangu ila nawalaumu nyie wanaume washenzi na mapanga yenu mnaowaingilia na kuwajaza mimba kisha mnawakataa. Mnagoma hata kuzihudumia hizo mimba mlizowajaza na wengine hata pesa ya kutolea hiyo mimba hawatoi eti mama yangu aitafute hiyo pesa ya kufanyia mauaji yeye mwenyewe.
Nikasita kuzungumza nikawatazama na sasa sikuweza kuyazuia machozi yangu, nikajifuta kidogo kisha nikaendelea kuzuingumza.
“Ni huyu ndiye mama yangu, mama ambaye kwenu mnamuita changudoa bila aibu mnamnunua, ni huyu huyu mnayemuita baamedi kila kukicha mnambughudhi kumshika sehemu zake nyeti hovyo na kumwagia bia zenu huku mkimtukana matusi ya nguoni, wengine mnafikia hatua hadi ya kumtukania mama yake… naam! Yule mama yake baamedi ambaye mnamtusi ndiye mama yangu, mmenijalia hapa na mapanga na marungu nazungumza nanyi viumbe mnaojipatia sheria mikononi, mnataka kumjua mama yangu wakati mama zangu mnaishi nao katika nyumba zenu mnawaita mahausgeli mnawanyanyasa na kuwaumiza sana nafsi zao, mama zao walikwishatangulia mbele za haki walitangulia pamoja na mama yangu lakini bado nina mama wengi sana duniani. Mama yangu ni yule mwanamke unayemuita mke wako kipenzi na kila siku unampiga bila huruma, mama yangu ni yule hawara yako mpumbavu anayejua kuwa umeoa nab ado anadai kuwa anakupenda, mama yangu ni yule binti wa miaka 18 nambaye bila aibu wewe mzee mwenye rungu na miaka yako 45 unashiriki naye mapenzi hivi wazazi wake wataajisikiaje umewahi kujiuliza?? Nasema na nyinyi mbona mpo kimya, nasema na nyinyi mama zangu nasema na nyiyi kaka zangu tuliozaliwa tumbo moja, nasema na baba zangu, nasema na wajomba na wadogo zangu… mkitaka kumjua mama yangu mnyanyue mikono yenu juu kisha mmwombe mwenyezi Mungu awarudishe katika matumbo mliyotokea kisha mzaliwe tena na huyo atakayewazaa NDIYE MAMA YANGU! Na baada ya hapo mkiishusha mikono yenu myashike mapanga na marungu yenu mniue mimi ndugu yenu. Naam! Natamani kufa ili nikaishia na mama zangu huenda huko ni sehemu sahihi zaidi….”……..
Nikashusha pumzi zangu kisha nikainama huku machozi yakiyafumba macho yangu, sikuweza kuona mbele na nilikuwa nimejiandaa kwa kila kitu!!
Baada ya dakika moja machozi yakiwa yamepungua niliunyanyua uso wangu juu, na sikukuta mtu zaidi ya yule mama aliyenihoji juu ya wapi yupo mama yangu!!
Nilishuka chini na kumfikia alikuwa amepiga magoti, nikamyanyua na kisha kumkumbatia.
Huku akiwa analia akaniambia maneno machache.
“Akiliamali kijana wangu naomba msamaha wako na ninaomba kuanzia sasa niwe mama yako wa hiari.”
Nilimkaribia zaidi na kumkumbatia yule mama na hapo nikamwambia WEWE NI MAMA YANGU!!!
JIFUNZE:
Ndugu yako si yule tu ambaye mnachangia damu ama tumbo moja. Bali ni yeyote yule ambaye anaweza kuwa nawe wakati wa machozi, kicheko.
Usisahau kushare post hii. Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasome


SIMULIZI FUPI: HUYU NDIYE MAMA YANGU MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA SIMULIZI FUPI: HUYU NDIYE MAMA YANGU MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA Reviewed by Love Psychologist on February 25, 2019 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.