WENGI wamejikuta kwenye majuto kwa kuwakabidhi watu wasiofaa mioyo yao. Wameambulia mateso makali, wamejikuta wamepoteza muda kwani wameachwa solemba wakati ambao hawakuutarajia. Ndugu zangu mapenzi yanauma. Yanauma kwelikweli hasa linapokuja suala la kumkabidhi mtu moyo wako ukiamini atakupenda, atakuthamini kama vile wewe unavyomthamini. Unakuwa na matumaini kwamba nipo na mtu sahihi. Mtu ambaye nitafanya naye maisha, mtu ambaye nitadumu naye katika shida na raha, mtu ambaye nitaingia naye kwenye ndoa mwisho wa siku anaingia mitini, inauma sana. Mapenzi ni uwekezaji.
Unawekeza nguvu, akili na maisha. Unapokuwa na mwenzi wako unamuamini. Unapanga naye mipango ya kufika mbali kwani kila ambaye anawaza maisha, lazima atakuwa anaifikiria ndoa na mtu sahihi. Atafikiria familia kwa maana ya kupata watoto, kusomesha na mambo mengine yahusuyo familia. Hiyo ndio safari ya wapendanao, inayoanzia kwenye urafiki, uchumba na hata baadaye ndoa.
Wahusika wanapoikamilisha safari hiyo pamoja huwa wanapongezana kwani si rahisi kwa kila uhusiano kuweza kuwa imara hadi kufikia hatua ya ndoa, ni kwa neema tu na baraka zake Mungu watu hujikuta wamekamilisha pamoja safari yao. Wengi sana hujikuta wakiishia njiani kwa namna moja au nyingine. Hii inatokana na sababu zifuatazo; Kuna ambao tangu awali wanaanzisha uhusiano na wenzi wao kutokana tu na mahitaji fulani, mathalani yawezekana akawa anafuata fedha au matamanio tu ya muda mfupi. Hana mapenzi ya dhati na mhusika. Matokeo yake, ataishi kwenye uhusiano kwa kipindi fulani halafu mahitaji yake yakiisha, anamuacha mwenzake solemba na kwenda kuanzisha uhusiano na mtu mwingine.
Msimamo; kuna wengine huwa wanakosa msimamo. Wanakuwa na tamaa. Anaingia kwenye uhusiano na mtu lakini baadaye anapokutana na mtu mwingine, mwenye mvuto au mahitaji yake mengine, anamhama mpenzi wake wa awali na kwenda kwa mwingine.
Kuna wengine wanayumbishwa na wazazi. Unakuta mwanamke anataka kuolewa, wazazi kwa sababu wanazozijua wao, wanamkataa muoaji. Au mwanaume anataka kuoa, wazazi wake nao wanamkataa Wapendanao huenda walishajipanga lakini wanajikuta wakishindwa kuoana. Ndoto zao za kufikia mbali zinafutika kulingana na matakwa ya wazazi, biashara inaishia hapo. Wengine ushirikina, kuna wengine wanajikuta wameachana kwa sababu tu ya ushirikina. Alikuwa anampenda mtu wake, anakutana na mtaalamu wa mambo ya kishirikina, anafanyiwa mambo na kujikuta amehamia. Kiukweli ni ngumu sana kumjua mtu ambaye si mwaminifu.
Inahitaji akili ya ziada na msaada wa Mungu kumtambua mtu ambaye upo naye kwenye uhusiano ni sahihi. Suala hili wanawake wengi wanaweza kulitolea ushuhuda. Ninavyoandika makala haya, najua wengi sana wameshazalishwa na kutelekezwa. Waliwapa wanaume mioyo yao matokeo yake wameambulia maumivu. Mwanaume anaishi na mwanamke na lake moyoni. Upendo unakuwa haupo kwa yule aliye naye. Au anayumbishwa na sababu nilizoziainisha hapo juu na matokeo yake anamuacha mwenzake. Nimekuwa nikisisitiza sana katika makala zangu na leo nitazidi kusisitiza. Usikubali kuanzisha uhusiano na mtu ambaye huna imani naye. Mchunguze kwa muda mrefu sana mtu kabla ya kumkabidhi moyo wako, kabla ya kufanya naye ngono zisizo salama ambazo zinaweza kukusababishia kupoteza ‘future’ yako. Ni kweli mtu anaweza kuficha makucha yake lakini si kwa miaka yote. Utamjua, ukigundua tu mueleze kwamba wewe si mtu wa mlengo wake. Achague moja, kubadilika au akuache umpate mtu sahihi. Muombe Mungu akuoneshe mtu sahihi. Fungua macho yako kumtambua kulingana na tabia zake, mapito yake na mwenendo wake. Mtu mwovu utamjua tu, muache mapema kabla safari yenu haijafika mbali.
ANAYECHEZA NA MOYO WAKO NI SAWA NA MUUAJI; UTAMJUAJE?
Reviewed by Love Psychologist
on
March 25, 2019
Rating:
No comments: