USALITI ni jambo baya katika uhusiano. Usaliti si ujanja japo wengi wanaowaza kusaliti huwa wanajiona wajanja.
Wanajiona wamewini pale ambapo wanasaliti na wenzi wao kutogundua kama wanasalitiwa.
Siku zote anayesaliti huwa anajiona mjanja kwamba, yeye anasaliti wakati mwenzake hasaliti.
Kwa asilimia kubwa, wanaume hujiona kama usaliti ni halali yao. Wanataka wao wasaliti lakini wapenzi wao wasithubutu kusaliti.
Kwa nini hawataki wenzi wao wasaliti? Wanaumia. Hakuna kitu kinachomchukiza mwanaume kama kusalitiwa. Kusaliti asaliti yeye, akisaliti mwenzake ni kosa la jinai. Anaona amedhalilishwa.
Anajisikia fedheha kwamba mpenzi wake amemuonaje? Amemchukuliaje? Hajakamilika idara gani? Anawaza sana. Anajiuliza jamii yote inayojua kitendo hicho inamtazamaje? Kwamba ni ‘boya’ kiasi gani hadi anaibiwa kirahisi. Jogoo hapandi mtungi? Hana uwezo kifedha?
Hapo ndipo unapokuta mwanaume anaamua kuchukua maamuzi magumu ikiwemo hata kuhatarisha maisha ya mwenzi wake.
Marafiki zangu, watu wanauana kwa sababu ya usaliti. Kwa mwenye penzi la dhati, kamwe hawezi kuvumilia usaliti.
Nikirudi katika mada yangu kama inavyojieleza hapo juu, kuna viashiria mbalimbali ambavyo ukiviona kwa mwenzi wako basi ujue unasalitiwa:
KUTOPENDWA KUCHIMBWA
Mara nyingi anayesaliti huwa hapendi kuchimbwa mambo kwa undani. Ana hofu anaweza kuchanganya madawa. Hupenda mazungumzo mafupi na moja kwa moja. Hapendi kuulizwa maswali mengi, ukimuuliza anayakwepa haraka na kutaka kukupeleka kwenye mazungumzo anayoyataka yeye.
Ukimuuliza kuhusu mipango yenu, ukimuuliza kuhusu mustakabali wa penzi lenu baadaye hukuondoa kwenye mstari na kukufanya usiwe na hamu ya kumuuliza mara mbilimbili.
HAPENDI UJUE RATIBA YAKE
Mara nyingi mtu ambaye ana lake jambo huwa hapendi ujue ratiba yake. Anataka usimzoee. Iwe anafanya maamuzi yake kulingana na yeye mwenyewe anavyojua.
Ikitokea unaijua ratiba yake, atakuwa ni mtu wa kutoa udhuru kila wakati.
Leo atakwambia kuna mgonjwa anakwenda kumuona. Kesho atakwambia kuna vikao na wafanyakazi wenzake. Siku nyingine atakuambia gari imepata pacha, analazimika kusubiri mafundi hadi wafike ndio aweze kuanza safari ya kurudi nyumbani.
Ukiona mtu ana visingizio vingi, jua kwamba njia zake si salama. Hataki ujue nini anafanya kwa wakati fulani. Kwa ambaye hana makando kando, anaeleza ratiba yake kwa uwazi. Hata kama inatokea dharura, anaieleza na inaeleweka.
SIMU YAKE KITUO CHA POLISI
Anayesaliti huwa hapendi kuuacha simu yake kiholela. Simu inakaa mfukoni kwake hata kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo. Mpo nyumbani, mpo kwenye mazungumzo ya kifamilia yeye simu yake ipo mfukoni.
Imetolewa mlio. Hataki uione maana inawezekana akatumiwa ujumbe, picha na mambo mengine ya kimapenzi.
HUCHATI SANA
Wanaosaliti wengi wao hupenda kutumia meseji katika mawasiliano yao. Hutumia njia hiyo kwa kuwa huiona ni salama sana kwao. Hapendi kupokea sana simu. Zaidi anapenda kuchati hivyo ni rahisi kuwasiliana na mchepuko wake.
HAKUTAMBULISHI NDUGU, MARAFIKI
Msaliti anataka usiwajue watu wake wa karibu. Anahofia wanaweza kuvujisha taarifa bila hata kujua wanauza silaha. Kuepuka hilo, anataka umjue yeye na watu wake wachache.
Zaidi sana atakutambulisha kwa rafiki yake ambaye ni mchepukaji mwenzake. Wanajua namna ya kucheza michezo ya usaliti.
USALITI HAUFAI
Kusalitiwa kunauma. Kuepuka maafa ni vyema wapendanao wakawa waaminifu. Kila mmoja akaheshimu hisia za mwenzake. Akamtunzia heshima, akawa na hofu kwamba akifanya hivyo anamuumiza mwenzake na kama ambavyo yeye ataumia akifanyiwa.
HIZI NDIZO SIFA ZA MABINGWA WA KUSALITI
Reviewed by Love Psychologist
on
March 19, 2019
Rating:
No comments: