Je, kuna dalili zozote zinazoashiria kutokea mfarakano katika ndoa yako? Kama hakuna, unafanya nini kudumisha maelewano mema baina yako na mwenzako. Kama kuna dalili za mfarakano, unafanya nini kuinusuru ndoa yako? Kwa hakika hakuna jibu rahisi la swali hili. Kama lingekuwepo jibu rahisi, leo kusingekuweko idadi kubwa ya ndoa zinazovunjika kila siku.
Suala la maelewano mazuri katika ndoa ni nyeti na huweza kukabiliwa na changamoto za aina mbalimbali. Aidha, wakati mwingine maelewano huathirika na kusababisha ndoa kuvunjika. Kila mara ninapozungumza na wanandoa kuhusu suala hili, walio wengi huonyesha wasiwasi kuwa huenda ndoa yao ikavunjika kutokana na kutokuwepo maelewano na maafikiano mazuri.
Sababu za kuvunjika ndoa huwa pamoja na wivu, kukosa uaminifu, kutoweka msimamo thabiti na tabia au mienendo isiyofaa na mambo mengine kadha wa kadha.
Mara nyingi hali ya kuharibika kwa maelewano wa mawasilano huanzia kwa mwanandoa mmoja. Wakati mwingine mwenzake kuweza hujitahidi kurekebisha hali hiyo na akashinda au kushindwa.
Kila mara ninapoandika kuhusu maelewano katika ndoa huwa nakumbuka kisa cha mwanamke mmoja jasiri aliyejitahidi kuokoa ndoa yake. Alikuwa akisumbuliwa sana mumewe mlevi. Kila siku alikuwa akirudi nyumbani usiku akiwa amelewa sana na kufanya vitendo visivyofaa kama kupanda kitandani akiwa amevaa nguo zake na viatu na wakati mwingine kukojoa sebuleni au chumba cha kulala, badala ya kwenda chooni. Kila wakati mkewe alipotaka kumvua viatu ili asichafue shuka na kumshauri aache tabia ya kunywa pombe kupita kiasi alimtukana na hata kumpiga hadi akaumia.
Tabia hii ilikuwa ilisababisha ugomvi mara kwa mara. Ingawa wazee walijaribu kusuluhisha, yule bwana hakuweza kujirekebisha hata kidogo. Siku moja alirudi mapema kidogo nyumbani akiwa amecharuka kwa ukali kuliko siku zote. Akaanza kumtukana mkewe na kumwambia kuwa amechoshwa na kero zake hivyo aondoke na kurudi kwao.
Alimwamuru aondoke na mtoto na akamruhusu kuchukua kila kitu anachokitaka pale nyumbani na kwenda nacho kwao. Alisisitiza kuwa aondoke na kama asipoondoka atampiga hadi kumjeruhi. Kwa kuwa alikuwa amelewa, mara akajitupa kwenye kochi na kusinzia fofofo. Akawa hajui chochote kinachotokea.
Kwa kuwa makazi ya kwao na yule mkewe yalikuwa katika mji ule ule akakodisha gari na kuomba msaada wa kumbeba mumewe na kumuingiza katika gari. Kisha akaondoka na mumewe na mwanawe hadi kwao. Alipofika akaomba chumba na kumlaza mumewe kitandani. Mumewe hakuamka hadi asubuhi kulipopambazuka.
Alipoamka akashituka kujiona yuko kwao na mkewe. Alipomuuliza mkewe akamjibu kuwa “Uliponifukuza kwako uliniruhusu nichukue kila kitu ninacho kitaka. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Katika nyumba yako hapakuwa na kitu chochote nilichokuwa nakipenda kukichukua na kuondoka nacho isipokuwa wewe. Ndiyo maana nimekuchukua ili tuje tuishi pamoja huku kwetu. Nimewaomba wazazi wangu waniruhusu kutumia chumba hiki kwa kuishi na wewe na mtoto wetu na wamenikubalia”.
Yule bwana akashangaa sana kwa lile jambo alilofanya mkewe. Akahisi moyoni mwake jinsi mkewe anavyompenda na kuhuzunika kwa jinsi alivyokuwa akimtendea hadi akamfukuza. Akamwomba mkewe msamaha na kumuomba warejee nyumbani kwao huku akiapa na kuahidi kuwa atajirekebisha wala hatamsumbua na kumkera tena. Hakika waliporejea yule mumewe akaacha kunywa pombe na kuongeza mapenzi zaidi kwa mkewe kuliko ilivyokuwa zamani. Wakaishi kwa furaha na starehe.
Kutokana na kisa hiki tumejifunza kuwa maelewano katika ndoa ni suala linalotaka busara na uvumilivu. Ndiyo maana suala hili linapewa uzito mkubwa katika saikolojia. Kuna nchi nyingi duniani ambako wanandoa watarajiwa hupewa mafunzo maalumu ya kuishi katika ndoa.
Kanuni zinazoweza kuwasaidia wanandoa kuepuka mfarakano
Kuna kanuni na taratibu nyingi zinazoweza kutumiwa na wanandoa ili kudumisha uhusiano, maelewano na ushirikiano katika ndoa. Baadhi ya kanuni hizo ni hizi;
1.Kutumia maneno mazuri
Imebainika kuwa maneno yana uwezo wa kuimarisha au kutia sumu katika ndoa, hata uhusiano wa kijamii na aina nyingine. Mara nyingi ninapoitwa kwenye mashauri ya wanandoa waliokosana hugundua kuwa mgogoro umetokana na wao kushindwa kutumia maneno mazuri. Kanuni hii inawaasa wanandoa kuwa kila anapozungumza na mwenzake atumie maneno yatakayomvutia na kumpendaze mwezi wake hasa hasa anapogundua kuwa jambo wanalolizungumzia huenda likasababisha ushindani.
Wakati mawasiliano yanapoonekana kuathirika vibaya na kwamba maneno ya kuzungumza ana kwa ana hayafikii maelewano yanayotarajiwa, mwanandoa anaweza hata kumwandikia barua mwenzake.
Kwa kawaida katika barua, anaweza kuchagua maneno ya kuandika kwa makini. Zamani katika nchi hasa za Asia wapenzi walikuwa wakitungiana mashairi au nyimbo.
Wakati mmoja niliwahi kuona barua ambayo bwana mmoja alimwandikia mkewe baada ya kuona uhusiano wao umeathirika na wanapozungumza ana kwa ana kunakuwa na ukungu unaofanya ujumbe unaokusudiwa umfikie mkewe, haumfikii vizuri na ndoa yao imo katika hatari ya kuvunjika. Barua hiyo ilikuwa hii:
Mpenzi Mke wangu
Daima huwa ninakushukuru kwa kunichagua mimi tushirikiane na wewe katika maisha yako.
Ahsante sana kwa uaminifu wako na uwazi. Naamini yote hayo unayofanya kwa ujasiri na uthabiti kwa ajili ya mapenzi yangu kwako.
Hata hivyo, mimi kama mumeo ninakutumaini kwa maisha yangu yote na nitafarijika sana iwapo kila mara utaongeza kuniashiria penzi lako kwangu kwa hisia na vitendo. Katika maisha haya hakuna chochote chenye thamani kubwa kwangu kama penzi langu kwako.
Nimekuandikia barua hii kukuthibitishia kuwa pamoja na changamoto zinayoyakabili mapenzi yetu katika ndoa, nitaendelea kukuhitaji katika uhai wangu wote. Nakuomba tuvumiliane na kuthaminiana siyo kwa ajili ya jambo jingine lolote, bali kwa ajili ya ndoa yetu. Mpenzi nakutaka na nakuhitaji kwa mapenzi ya kudumu.
Mumeo.
Barua hii ilimsaidia huyu bwana aliyeindika kufikisha kwa mwanandoa mwenza ujumbe uliomfanya hisia zake kuhusu ndoa yao zistawi na kuleta matokeo mazuri zaidi.
Itaendelea wiki ijayo...
2. Kumsifu mwenzako
Kumsifu mwanandoa mwenzio kila anapofanya jambo la kupendeza, ni kitendo kinachomfariji na kumpa imani kuwa unampenda na kumthamini. Ili sifa iwe ya kufaa na inayotimiza malengo yanayokusudiwa, haina budi itolewe katika wakati mwafaka na itolewe katika manma bora inayofaa. Baada ya kumwelewa vyema mwenzio ni vyema ujiulize ni wakati gani ingefaa zaidi asifiwe na ni njia ipi iliyo mwafaka zaidi kwa tukio fulani na mahali fulani. Baada ya kupata majibu ya lini umsifu, huna budi kumsifu katika namna inayoonyesha hisani ya upendo. Sifa inaweza kuwa ya kumpa moyo, kumpongeza au kumwonyesha imani uliyonayo kwake.
3.Epuka kulaumu
Unapomfahamisha mwenzio kuhusu kosa alilofanya, mweleze kwa utulivu wala usimshambulie au kushinikiza kwa kumbebesha lawama nyingi kwa makosa. Badala ya kusisitiza kosa mweleze mwenzio tatizo na wala usimshutumu kwa kuwa unaweza kumfanya azipokee lawama zako kwa kujihami, hali ambayo huweza kuelekea katika msutano na ubishi na pengine ugomvi.
4. Epuka kufedhehesha au kutukanana
Tabia ya kutukanana na kufedheheshana ni sumu ya uhusiano na ushirikiano wa aina zote. Wanandoa hawana budi kuiepuka kwa kila hali. Kwa kawaida huwa haina matokeo mazuri kwani huweza kuwafanya wanandoa wakatupiana matusi ambayo huzaa ugomvi unaweza kuwafarakanisha na pengine hata kufanya ndoa ivunjike.
5.Usitafute suluhu ukiwa umekasirika
Kunapotokea mtafaruku baina yako na mwenzako uliokufanya ukasirike, haifai kujaribu kujadili suala hilo ili kutafuta suluhu wakati ungali na chuki. Kwa kawaida hasira huwa haiwezi kumwongoza mtu kufanya uamuzi sahihi. Wakati mwingine hasira huweza kuvuruga zaidi na kufanya mtafaruku kuwa mkubwa zaidi. Ni vyema ufanye subira hadi hasira yako itakapotulia ndipo ufanye majadiliano na mwenzako ya kutafuta suluhu.
6.Kumuhami Mwenzako
Kumuhami mwenzako ni kumwangalia na kumtunza. Kutunza katika maana hii ni kama ile inayokusudiwa na methali isemayo “Chanda chema huvishwa pete” Hivyo, huna budi kila inapobidi kumpatia mwezio kitu chochote anachohitaji na ambacho akikikosa kitamwathiri kwa kiwango fulani. Vitu hivyo ni vile vya matumizi yake binafsi na siyo vya matumizi ya familia. Siyo lazima ungoje mpaka akuombe. Vitu hivi ni hidaya yaani kitu unachompa mtu kama ishara ya mapenzi
7.Mwambie mwenzio unampenda
Watu wawili wanapokuwa wapenzi huwa hawaishi kuambiana kuwa ‘Nakupenda’ na kuitana majina matamu. Wanapooana wakawa mume na mke, walio wengi, huendelea kufanya hivyo kwa miaka michache tu na kisha kuacha. Ili kuimarisha uhusiano hawana budi kuendelea kufanya hivyo. Kila mara unapomwambia mwenzi wako unampenda na ukataja sababu za kumpenda unajenga imani inayoimarisha upendo katika ndoa. Tukumbuke kuwa kila mwanandoa anaposikia sauti ya mwenzake akisema “Nakupenda mke/mume wangu” kwake hiyo huwa sauti nzuri kuliko nyingine zote.
8.Usijidhili nafsi yako
Mwenzi wako katika ndoa asipokutekelezea baadhi ya mambo yanayompasa, usikasirike na kuhuzunika kimya katika nafsi yako. Baadala ya kukasirika na kumlaumu mwenzako na pengine kuwaza kuwa anafanya kusudi, mweleze kwa hekima na busara ili akutimizie. Huenda ukagundua kuwa wala hakuwa akijua kama anatakiwa kumfanyia mwenzake mambo hayo.
9.Usiseme uongo
Katika maisha wakati mwingine mtu kuweza kusema uongo kwa sababu maalumu. Lakini siyo vyema kumdanganya mwezi wako wa ndoa. Wakati wowote atakapogundua kuwa umemdanganya atakasirika na kupunguza imani yake kwako. Jambo hili likiendelea mara kwa mara linaweza kumfanya mwenzako akakosa imani kwako. Hali hii itaathiri zaidi ndoa na pengine kusababisha matendo au matukio yanayoweza kuwafanya wanandoa wafarakane na hatimaye pengine ndoa kuvunjika.
10.Kuwa na fursa ya kuwa wawili pekee
Mshauri mwenzako muwe na utaratibu wa kutoka na kwenda mahali ambapo mtaweza kuwa wawili mbali na vitu vyote vinavyoshughulisha akili. Mnaweza kuwa mkitoka kama hivyo mara moja kwa wiki au kwa mwezi. Utaratibu huu utawasaidia kupumzisha akili na kupata fursa ya kuzungumza yaliyo katika nyoyo zenu na kupanga mipango ya maisha yenu.
11.Usifanye maamuzi peke yako
Katika ndoa kuna mambo mengi yanayohitaji uamuzi na mwengine ni ya msingi sana. Kila mwanandoa hapaswi kufanya uamuzi peke yake. Anawajibika kumshirikisha mwenzake katika kujadili na kufanya maamuzi kwa kila jambo hususwani linalowahusu wote.
Moja katika mambo muhimu sana katika maisha ya binadamu akiwa mwanaume au mwanamke ni kuweza kuishi vyema katika ndoa. Hakuna jambo baya kama watu walio katika ndoa kushindwa kudumisha mapenzi na hali ya kuelewana na kushirikiana. Katika makala hii tumejaribu kueleza baadhi ya mambo ambayo yataweza kuwasaidia wanandoa kuimarisha maelewano katika ndoa.
Je unatambua jinsi ya kuepuka mifarakano katika ndoa?
Reviewed by Love Psychologist
on
March 18, 2019
Rating:
No comments: