Niliingia kwenye ndoa na mume wangu mwaka 2010, nilikua nampenda sana, pamoja na kwamba nilikua nikimfumania mara kwa mara lakini niliamini kuwa kama akinioa basi atabadilila na tutakuja kuishi kwa amani. Lakini haikua hivyo, wiki moja tu baada ya ndoa nilifumania meseji akichat na mwanamke mwingine, alionekana kama ni mwanamke mpya kwani ndiyo kwanza alikua anamtongoza na akimuambia kuwa hajaoa.
Nilikasirika sana na kuchukua namba ya yule dada, nilimuambia kuwa yule anayechat naye ni mume wangu tena wa ndoa na kama anamuambia hajaoa basi anamdanganya. Jioni mume wangu alirejea, alinipiga sana akinishutumu kwa kumdhalilisha, akiniambia nikwanini nahangaika na simu yake, alinipiga marufuku kugusa simu yake na kuniambia yeye ndiyo mwanaume na hawezi kuendeshwa endeshwa na mwanamke.
Kwakua ndoa ilikua changa niliendelea kuvumilia, sikuongea kwa mtu yoyote, lakini wakati nikiwa na ujauzito wa mtoto wetu wa kwanza kuna mwanamke alikuja katika nyumba tuliyokua tukiishi, alikuja kama mpangaji tu wa kawaida, lakini baada ya muda niliona kama mume wangu kabadilika, anawahi kurudi nyumbani lakini anatoka na kwenda kwa yule dada, alikua akiniambia wamezoeana tu ni majirani.
Nilichunguza na kuja kugundua kuwa ni mchepuko wake na alikua mapangia nyumba pale jirani na mimi ili asipate shida kumtafuta. Niliumia sana, nilijaribu kuongea naye lakini niliishia kupigwa akiniambia kuwa namchinganisha na majirani, alikataa katakata kuwa anatembea naye huku akiniambia kuwa siwezi kumzuia kuchat na majirani wala kuwatembelea kwaajili ya wivu wangu.
Hali ile ilinichosha na kuamua kuwaambia nyumbani, nilimuambia Mama ambaye aliniambia vumilia. Aliniambia “Kwa hali yako hiyo nilazima mume wako atachepuka, ushauri wangu ni wewe kurudi kulinda ndoa yako. Kama ukitaka kuondoka utamuchia huyo mwanamke mwanaume na hutajenga bali utabomoa.” Nilirudi kwa mume wangu na kuamua kukaa kimya nikipambana ili kulinda ndoa yangu, nilijirahidi kumfanyia mume wangu kila kitu lakini hakuridhika bado aliendelea na yule dada.
Nilipojifungua niliona ila hali inazidi kuniumiza, nilikua naumia kwani yule dada alikua akinitukana, kunisimanga na kama nikiongea niliishia kupigwa. Siku moja nilikua nimekaa nnje na mwanangu, Dada yangu mmoja alikuja kunitembelea, yule dada alikuja, akamsalimia dada lakini mimi hakunisalimia, sikujali lakini alikaa pembeni yangu na kuchukua simu akaanza kuongea na mume wangu, alikua akimuagiza vitu vya kumletea tena akimtaja kwa jina la mwanangu.
Niliumia sana, uzalendo ulinishinda, nikampa mtoto dada yangu na kuanza kugombana naye, tulishikana nusu kupigana lakini watu wlaikuja na kutuamulia. Nilirudi ndani lakini mume wangu alikuja na kuniambia kuwa hawezi tena kuishi na mimi kwani siwezi kuishia na majirani. Alinitukana sana matusi mengi ya nguoni, alinifukuza akimchukua mtoto, kipindi hicho mwanangu alikua na miezi sita.
Alimchukua na kusema siwezi kumlea mtoto vizuri hivyo nimuachie mwanangu na yeye atalelewa na huyo dada. Nilihisi kuchanganyikiwa, nililia na kulia lakini hakujali, alinifukuza na mtoto akachukua. Baada ya kunifukuza kabla ya mimi kufika nyumbani alipiga simu kwa ndugu zangu na kuwaambia nimekimbia na kutelekeza mtoto, akamuambia Mama yake ambaye alinipigia simu na kunitukana, nilitukanwa sana, niliporudi nyumbani nilijaribu kuwaelewesha na kuwaambia ukweli lakini hawkaujali.
Mume wangu ni wale wanaume ambao mbwele za watu ni wakimya, wanajali framilia, wanahudumia kila mtu na kila kitu wanakifanya vizuri. Ni watu wa Mungu hivyo mimi nilionekana mkorofi. Nyumbani walinilazimisha kurudi kwa mume wangu, lakini sikua tayari kwani mume wangu mwenyewe nikiongea naye kwa simua alikua akiniambia kama nikirudi kwake basi ataniua. Nilibaki nyumbani ambapo napo walikua wakininyanyapaa, kwani kwa kiasi kikubwa mume wangu alikua akiwasaidia lakini baada ya mimi kuondoka alikata mawasiliano.
Nilikaa nyumbani kwa miezi miwili bila kumuona mwanangu, lakini siku moja mume wangu alikuja nyumbani, alikuja kambeba mtoto eti anapiga magoti kuniomba msamaha, ananiomba si kwakua kanikosea, hapana nikwakua anasema amechoka kulea familia peke yake.
“Sijui kama nimekukosea wapi, najua hunipendi, ila fikiria familia yako eliza, fikiria mwanao bado mdogo anateseka, rudi unisaidie kule. Hata kama mimi hunitaki, mchukua mtoto hata umnyonyeshe, mtoto bado mdogo sana kunywa maziwa ya Ng’ombe.”
Aliongea mbele ya ndugu zangu, kwa namna alivyokua akiongea ni kama vile mimi ndiyo nilikua simtaki na ananibembeleza kurudi. Ndugu zangu walinishupalia kurudi, hata dada yangu yule ambaye alikua nyumbani wakati ugomvi unaanza aligeuka na kuwa upande wake. Nililazimia kurudi kwa mume wangu, ile kurudio nikagundua kuwa kumbe yule dada aliondoka pale, alishindwa kulea mtoto na kukimbia nyumba.
Mume wangu alibaidlika kwa mwezi mmoja tu, lakini akarudia tabia zake zilezile, sasa hivi alianza ulevi, akawa anatembea na mabaa medi na kila nikiongea aliniambia kama sitaki niondoke kwani nitarudi tu. Alikua akinikumbusha kuwa hata ndugu zangu wapo upande wake kwani kwao yeye ni mwema. Alikua akinipiga mara kwa mara, nilipata ujauzito wa pili,a linipiga mpaka mimba ikatoka, alitangaza kwa wamtu kuwa nimetoa mimba yake.
Ilikua mimba kubwa ya miezi mitano, kila mtu alikua anajua, alinitangaza sana akisema nina wanaume wengine ndiyo maana sitaki kuzaa naye. Niliumia sana kwani hata Mama yangu mzazi alianza kumuamini, alianza kutilia shaka mambo niliyokua nikimuambia, tuliendelea kuishi hivyo, mimi nimsomi lakini alinikataza kufanya kazi, alikua akiniambia hataki nifanye kazi atanifungulia biashara.
Lakini mbele za watu alikua akijitangaza kuwa mimi sitaki kujishughulisha, alikua ananifungulia biashara kweli lakini kila mara akishanifungulia biashara basi huacha kutoa matumizi, ananiambia pesa zote za matumizi nichukue dukani, duka likifa basi husihia kunitukana, kunitolea maneno ya kashifa na kusema kuwa nammalizia pesa zake kwa kuhonga wanaume, alishanifungulia maduka matatu na yote yalikufa.
Mwaka 2016 nilipata ujauzito wa tatu, panmoja na vipigo vyake lakini nilivumilia mpaka kujifungua. Alionyesha furaha kwa muda mfupi, lakini mwanangu akiwa na miezi sita, mwaka 2017 katikati, aliondoka na kuanza kuishi na mwanamke mwingine, alikua ni Mama mtu mzima, yule Mama alikua ni bosi wake, mume wangu mimi anafanya kazi benki na yule Mama alikua ni meneja wa benki moja kubwa tu hapa nchini, walianisha mahusiano, yule Mama amabye ni mke wa mtu alikua akimcontroll sana mume wangu.
Mama alikua na mume lakini ndoa yao ina migogoro, mume wake ni mtu wa wanawake, mtu mkubwa tu, anampiga mara kwa mara hivyo alimtumia mume wangu kujipoozea. Mume wanyu alilowea huko hata matumizi alikua akituma kwa shida, nilikua naumia na kulia kila siku. Nyumbani hakukua na mtu wa kunisaidia, hakuna mtu aliyeamini kuwa mume wangu anaweza kufanya yote hayo, kila mtu alisema kuwa namsingizia.
Mwaka 2018 mwanzoni nilikutana na Makala yako moja Kaka, kuna dada alikua na kisa ambacho kimefanana na changu, ulimuambia ukweli kuwa tatizo ni yeye na si mwanaume. Ulimuambia kama mwanaume anamfanyia upuuzi uleule kila siku na bado anavumilia basi yeye ndiyo anapaswa kubadilika. Ulimuambia ana mikoni miwili, miguu miwili, kichwa na akili kwaninia lie unyonge na kumlaumu mwanaume wakati huyo mwanaume hampi pumzi.
Niliamua kununua vitabu vyako vyote viwili, nilisoma na kukupigia simu ukaniambia nilazima niamue kuwa na furaha yangu mwenyewe na kwa mtaji wowote ule nilazima nifungue biashara hata kama ni ya maandazi. Baada ya kuongea na wewe na kujadiliana na wewe kuhusu aina ya biashara ya kufanya ulinishauri kutokana na eneo langu basi nifungue biasjara ya matunda. Kweli nilifanya hivyo, nilikua nauza matunda ya rejareja, lakini hayakulipa.
Nilirudi ukaniambia nisiuzie pale nyumbani kwani inaonekana pamoja na kuwa hakuna sehemu yanauzwa lakini watu wa hapo si watu wa kumuunga mtu mkono. Nilihama na kwenda sokoni, mume wangu aliposikia alikuja kufanya fujo na kuniambia anataka kuwachukua watoto kwani nawatelekeza na dada wa kazi. Aliniambia kama nataka kubaki na watoto nibaki nyumbani atanihudumia. Nilitaka kukubaliana naye lakini baada ya kukupigia uliniambia niache ujinga kwani hatanihudumia.
Uliniambia anaona nafanikiwa siwezi kuwa mfungwa wake hivyo nisijali kama atawachukua. Uliniambia hata yeye watoto ni wake, hawezi kuwapa sumu, nimuambie kama anawachukua basi awachukue, aliwachukua kweli, niliumia lakini ukaniambia nitafute pesa kwanza ndiyo nikawachukue wanangu kwani hata nikiacha kufanya biashara haitawasaidia watoto. Nilimuacha akwachukua, sikumuuliza chochote, aliwapeleka kwa Mama yake na kuendelea kutukana kuwa nimewatelekeza.
Nikiwa pale sokoni nilipata dili la kuchukua Nazi mtwara na kuleta Dar, uliniambia natakiwa kuhamishia hasira zangu za kunyang’anywa mtoto katika biashara. Nilikua na mtaji kama wa laki tano hivi, lakini mtu aliyenipa dili aliniambia niende niwe namkusanyia nazi zake na yeye atakua ananilipa. Nilikubalia na kwenda kukusanya nazi, nilikua nakaa Mtwara hata wiki tatu nakusanya na mletea, huko nilikua najikusanyia mtaji wangu kidogo kidogo. Katika miezi mitatu niliweza kupata kama milioni mbili za kwangu.
Hapo nilianza kununua mzigo wangu, kuna dada mwingine nilikutana naye akaniambia kuwa kuna dili Dodoma, nikaanza kupeleka nazi huko. Nilijikusanya mpaka nimeweza kuwa na mtaji wa Shilingi milioni tatu na kupanga vyumba viwili. Mume wangu baada ya kuona mambo yananiendea vizuri na sijali kuhusu watoto aliwarudsiha wanangu, mwanzo alidhani ananikomoa, anarudi na kuniomba msamaha, ananiambia anataka turudiane nilee familia.
Pamoja na kuomba msamaha lakini bado anaishi na yule mwanamke kwani kwa sasa mume wa huyo mwanamke kashamtelekeza na hawana mawasiliano, bado wana ndoa ya kanisani lakini hawana mahusiano. Nimemuambia amuache kwanza huyo mwanamke lakini ananiambia atamuacha taratibu kwani kuna vitu vingi ambavyo amemfanyia, amenihakikishia kuwa atabadilika na hivyo vitu vikikamilika atamuacha mazima.
Ameenda kwa ndugu zangu na kuwaomba waongee na mimi ili turudiane, mimi bado nina wasiwasi. Najua Kaka Iddi umeshaniambia kuwa habadiliki na kama nikirudi basi atanitia umasikini na kunitelekeza lakini bado inauma, naomba upost kisa changu nipate maoni ya wengine. Bado nampenda mume wangu na naamini labda nayeye ananipenda ndiyo maana kashindwa kunisahau lakini nawaza je atabadilika au anataka kuniumiza tena kwakua tu nina biashara na nina maisha yangu ambayo hayamtegemei yeye? Naombeni ushauri wenu nimechanganyikiwa sijui nifanye nini ninusuru ndoa yangu?
NIFANYE NINI ILI KUINUSURU NDOA YANGU? BADO NAMPENDA MUME WANGU!
Reviewed by Love Psychologist
on
March 08, 2019
Rating:
No comments: