Siku zote fungua milango kwa watoto kufurahi nyumbani kwako na watoto wenzao na utawasaidia kuepuka mengi kwa dunia ya sasa yenye changamoto za kila namna. Utajua wanacheza michezo gani, wanaongea lugha gani na kujua tabia zao kiundani zaidi. Huu ni mwanya mzuri kwa mzazi kumfundisha mwanao na marafiki zake kile unachoona ni sahihi na pia kuwarekebisha pale wanapokosea.
Ni vyema mtoto akawa huru kuchagua rafiki wa kucheza naye shuleni na hata nyumbani. Wewe kama mzazi / mlezi unaweza kumsaidia ushauri tu juu ya marafiki wema wenye maadili mema kama wewe ulivyojitahidi kumfundisha. Tumia muda wawapo hapo kwako kusikiliza mazungumzo yao, michezo na tabia za marafiki aliowachagua mwanao kisha umshauri kuhusu marafiki hawa endapo utaona sio rafiki wazuri na mpe heko unapoona marafiki zake ni binadamu wema.
Ni vyema pia ukayafanya makazi yako kuwa sehemu rafiki kwa marafiki wa watoto wako kujumuika na kufurahi pamoja. Hii itakusaidia kujua tabia za marafiki hawa na pia itasaidia kuwaweka salama watoto wako kwa sababu watacheza na kufurahi nyumbani kwako na sio sehemu zingine usizofahamu. Mara nyingi watoto wako wasipowaalika marafiki zao nyumbani kwako yawezekana wewe ni mkali sana, hauwapi uhuru wa kuchagua marafiki wanaowataka wao ama hapana mazingira rafiki ya wao kujumuika.
Ukichunguza kwa makini zile familia ambazo nyumba zao ni ‘vijiwe’ vya marafiki wa watoto wao utagundua kuwa wazazi wanawajali marafiki wa watoto wao. Wanawakarimu. Mathalani hata zawadi wanazowanunulia watoto wao kama mipira, nk. zinatumika pamoja na marafiki zao. Ukiweza, wajumuishe marafiki za watoto wako hata kwenye mitoko yenu ya kifamilia.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
UKWELI MTUPU: Pafanye nyumbani kwako ‘kijiwe’ cha marafiki wa watoto wako
Reviewed by Love Psychologist
on
March 09, 2019
Rating:
No comments: