Sponsor

banner image

recent posts

Ijue dawa ya mpenzi msaliti


HAKUNA asiyejua uchungu wa kusalitiwa. Kusalitiwa kuna maumivu makali sana. Kwa kawaida usaliti huwa unauma hata kama hujamfumania mpenzi wako moja kwa moja. Kukiwa na mazingira ya mpenzi wako kuwa na mtu mwingine moyo huenda  mbio na furaha hutoweka!

Ukishindwa kudhibiti hisia zako, inaweza kukusababishia kushindwa kutimiza majukumu yako ya kila siku vyema. Usaliti ni tatizo kubwa sana rafiki zangu. Lakini vipi, umeshawahi kufikiri juu ya kugundua kabisa kwamba unasalitiwa?
Umewahi kufikiria…unampigia simu mpenzi wako, halafu anapokea mtu wa jinsia nyingine tena usiku wa saa sita nini kinatokea? Mathalani umekwenda kwa mpenzi wako usiku kwa kumshtukiza, halafu unamkuta yupo na mtu ndani, utaumia kiasi gani?
Hata hivyo, maumivu siyo mwisho, machozi yako siyo suluhisho, lazima uende hatua moja zaidi ya hapo. Haya ni mambo ambayo yanaweza kutokea katika uhusiano, umejiandaaje? Umegundua wazi kuwa mwenzako anakusaliti, unajua unapaswa kufanya nini? Au wewe unadhani ungefanyaje?
Je, ungejiua?  Ungeachana naye? Yote hayo siyo suluhisho la kudumu. Kote huko kuna matatizo yake, lazima upate suluhisho moja la kumaliza kabisa tatizo hili.
Nimekuwa nikitoa ushauri kwa watu wengi sana kuhusu masuala ya mapenzi, ndoa  na elimu rika. Siku moja nilipokea simu ambayo ndiyo iliyonisukuma hasa kuandaa mada hii. Ilikuwa ni simu kutoka kwa mama mmoja ambaye alilalamikia kuhusu kusalitiwa na mumewe.
Katika mazungumzo yetu, alisema: “Mimi ni mama mwenye watoto wanne, naishi na mume wangu kwa miaka 15 sasa, mume wangu si mwaminifu na nimegundua kwamba anatoka nje ya ndoa yetu tangu mwaka 2004.
“Lakini kila nikimuuliza anakuwa mkali, wakati mwingine hunipiga au kunipeleka nyumbani kwa ndugu zake. Baadaye alikwenda kusoma kozi fupi ya miezi sita, aliporudi akaanza tena tabia yake ya kurudi nyumbani usiku, wakati mwingine hadi saa sita!
“Ninapompigia simu usiku akiwa amechelewa, anasema yupo ofisini. Lakini kuna siku nilimuomba simu yake, nikaanza kupekua meseji, nikakutana na sms chafu, nilipomuuliza juu ya sms zile, akasema kama anataka aniambie ukweli, basi nimuahidi kumsamehe.
“Kwakuwa nilikuwa nataka kujua ukweli, nikamwambia nitamsamehe, ndipo aliponiambia kwamba zile meseji zilikuwa za dada mmoja hivi (nahifadhi jina lake) jirani yetu na alikiri kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.
“Sikufanya fujo yoyote, hadi leo sijamwuliza chochote, lakini nataka kuachana naye ili niangalie maisha yangu maana tabia yake ya kurudi nyumbani usiku bado hajaacha. Tangu tuoane sijawahi kumsaliti hata siku moja na wala sitarajii kufanya hivyo.
“Sitaki mwanaume yeyote kwa sasa, natamani kuishi mwenyewe. Naomba ushauri wako kaka Shaluwa. Kichwa hakifanyi kazi sawasawa, pia sina raha katika ndoa zaidi ya kero tu! Nisaidie tafadhali kaka yangu.”
Hayo ndiyo maneno ya dada yetu huyo ambaye kwake, maisha ya ndoa ni machungu kuliko kawaida. Ni imani yangu kwamba, wapo wengine wenye matatizo kama ya huyu dada.
Wiki moja baadaye niliandika mada iliyotoka katika gazeti damu moja na hili la Risasi Mchanganyiko ambapo nilimshauri yule dada moja kwa moja. Yawezekana na wewe upo katika tatizo kama la dada yetu huyo, huna haja ya kulia na kuhangaika. Ipo dawa.
Kwa faida ya wote, wenye tatizo kama hilo na hata wale ambao hawana, lakini kwa sababu wote tupo kwenye sayari ya mapenzi, inawezekana kabisa yakakukuta. Sasa hapa tutapata darasa.
Ushuhuda huu uwe utangulizi kwako katika kusoma kwa upana na kujifunza zaidi juu ya usaliti.
TATIZO LIKO WAPI?
Kwanza kabisa nilimwambia huyo dada kuwa anakosea sana kuwa na suluhisho la moja kwa moja, wakati akiomba ushauri. Hana sababu ya kukata tamaa na kuwa na wazo la kuachana na mume wake.
Kubwa zaidi ambalo anatakiwa kuwaza kwasasa ni kwamba, tayari ameshaingia kwenye ndoa, kama inavyojulikana ndoa haina majaribio ni ahadi. Sasa siyo rahisi kuamua kumuacha mumewe.
Hutakiwi kuwa mvivu wa kufikiria kiasi hicho, unatakiwa kuwaza mbali zaidi ya hapo. Unasema umechoka, ni sawa…hakuna anayeweza kuzoea kusalitiwa, lakini ni kweli kwamba umeshindwa kukabiliana na tatizo hilo la mumeo kukusaliti?
Siku zote matatizo hayakimbiwi, hutafutiwa suluhisho ili baadaye uweze kusimama kifua mbele ukifurahia mafanikio yako baada ya wewe mwenyewe kuibuka mshindi!
Mimi nina mtazamo tofauti kidogo kuhusu usaliti, siamini hata kidogo kwamba mwanaume/mwanamke anaweza kumsaliti mwenzi wake kwa ‘makusudi’, lazima kuna kitu fulani nyuma ya pazia. Hebu jiulize, mumeo alikuwa anakusaliti tangu mwanzo wa uhusiano wenu au ni tabia mpya?
Umesema kwamba upo kwenye ndoa kwa miaka 15 sasa na mnao watoto wanne, je, ni kweli kuwa kwa muda wote huo mumeo alikuwa anakusaliti? Naamini jibu litakuwa si kweli.
Niliamua kumshauri hivyo gazetini, nikiamini kwamba kuna wengine ambao wangejifunza kupitia yeye. Ndivyo ilivyokuwa, mara baada ya gazeti kutoka, wasomaji wengine wengi waliwasiliana na mimi, wakieleza matatizo yao lakini wengine wakitoa michango yao ya ushauri.
Hebu tuone baadhi ya maoni hayo, nina hakika kuna kitu utajifunza, kisha tutaendelea na mada yetu.
Msomaji wa kwanza: Rejea makala yako gazetini, hakuna dawa ya kusalitiwa, unatia hasira sana, mume wangu alikuwa anatembea na rafiki yangu kwa muda mrefu sana, una dawa gani hapo? Nina maamuzi, najipanga, nitaachana naye baada ya kuweka mambo yangu sawa. Kuwa mwangalifu na unachokiandika. Maumivu mengine hayana dawa. Usidanganye watu!
TUNAJIFUNZA NINI?
Kwanza nilishtuka sana baada ya kupata hii meseji kutoka kwa msomaji huyo, lakini baada ya kutulia kwa muda nilitabasamu! Unajua kwa nini? Kwa sababu niliona nimefanikiwa kugusa pale nilipokuwa napataka!
Pole sana dada yangu, najua ni kiasi gani unateseka na usaliti, lakini naamini kabisa, mpaka mumeo anafikia hatua ya kutembea na rafiki yako kuna mahali unakosea bila wewe kujua.
Kwa haraka-haraka, kwa kukusaidia wewe na wengine wenye tatizo kama lako, usiruhusu mazoea ya karibu sana kati ya mumeo na shoga yako. Hata wanaume pia, msiruhusu rafiki zenu wawazoee sana wake/wapenzi wenu. Mazoea kupitiliza ni hatari. Yanaweza kuwaingiza mtegoni.
Ikiwezekana hata namba za simu wasibadilishane. Wanataka kuwasiliana kivipi? Kwa ajili ya nini mtu na shemeji yake? Abiria anachunga mzigo wake mwenyewe jamani! Hata hivyo, kuna baadhi ya vitu ukivikosea utasalitiwa tu, hata kama si kwa rafiki yako kuna nyumba ndogo!
Tena kwa mumeo huyo ambaye amefikia hatua anatembea na shoga yako, bila shaka atakuwa na msururu wa wanawake huko nje.
Unajua nini kilitokea? Baada ya kuandika mada hii kwa mara ya pili, msomaji huyo alinipigia simu na kuniambia amebatilisha maneno yake. Kwamba amebadilika na amejifunza kutokana na mada hii. Akili yake imekuwa mpya na ameshayaondoa mawazo ‘mgando’ aliyokuwanayo awali.
Kwangu mimi, naona alifanya maamuzi mazuri, yenye busara na bila shaka sasa anaishi akiwa na mtazamo mpya kabisa. Kwako pia liwe funzo.
Ijue dawa ya mpenzi msaliti Ijue dawa ya mpenzi msaliti Reviewed by Love Psychologist on March 24, 2019 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.