Sponsor

banner image

recent posts

NILIMFUMANIA MUME WANGU NA MDOGO WANGU WA DAMU AKANIPIGA KWA KUMFUMANIA!






Mwaka jana nilikua katika hali mbaya kabisa katika maisha yangu, nilimfumania mume wangu na mwanamke mwingine, tena si mwanamke tu, nilimfumania na mdogo wangu wa damu, tumbo moja toka ni toke. Walianzisha mapenzi, tena si kwakua nilikua nikiishi na mdogo wangu nyumbani hapana, hata kunitembelea alikua hanitembelei mara kwa mara, nilipigiwa tu simu na mtu kuwa mume wangu yuko na mwanamke mwingine nilipofika nikakuta ni mdogo wangu.

Aliponiona hata hakupaniki, alianza kunipiga kwa kunifumania, mdogo wangu alinitukana na kuniambia kuwa mimi siwezi ndoa, yeye anampa kila kitu ndiyo maana mwanaume kaja kwangu. Nilikua nimechanganyikiwa kwakweli, nilishindwa hata chakuongea, nilitamani kwenda nyumbani kuwaambia, nilitamani kunywa sumu na nilitamani mambo mengi sana lakini yote niliogopa kuyafanya.

Nilirudi nyumbani kumsubiri mume wangu kuja kuomba msamaha lakini hakuja, alikaa kama wiki moja hivi. Ilinibidi mimi kumtafuta kwani ndani kulikua hakuna kitu, kipindi hicho nilikua ni Mama wa nyumbani hivyo hata kununa nisingekua na uwezo wa kununa muda mrefu. Nilimpigia simu na kumuambia kuhusu watoto, aliniambia kuwa sina adabu nimuombe msamaha kwa kumfuatiliafuatilia.

Nilikata simu kwa hasira kwani niliamini yeye ndiyo anapaswa kuniomba msamaha kwa kila kitu. Hasira zilipoisha ndipo nikakumbuka kuwa watoto bado wanahitaji kula. Nililazimika kujishusha, nikaomba msamaha na ndipo alinitumia Shilingi elfu kumi. Sikua na namna zaidi ya kushukuru, hakurudi mpaka siku tatu baadaye. Alirudi kana kwamba kulikua hakuna kitu kimetokea, alijifanya kunilaumu kwa kuchepuka kwake na kuniambia kama ningekua najitunza kama mdogo wangu basi asingenisaliti.

Nililazimika tena kuomba msamaha, nilijikuta nakua kama mjinga kwani sikua na namna. Nisingeweza kurudi nyumbani kwani kwanza uwezo wa kifedha ni mdogo kwa wao kunipokea na wanangu wawili, lakini pili hata kama ningesema nini hakuna mtu ambaye angeweza kuamini kuwa mume wangu anaweza kunisaliti. Sanasana mimi ndiyo ningeonekana kama mkorofi, namsingizia na nataka kumharibia jina, ningeweza kufukuzwa.

Nililazimika kunyamaza kimya, sikuweza kumuambia mtu yeyote. Niliteseka na kile kitu kwa muda wa miezi mitatu, nilijikuta nakonda, najichukia na manyanyaso ya mume wangu yalizidi, kila wakati alikua akiniambia mimi mbaya, ananivumilia tu, alikua akinipiga na kuniambia mimi ndiyo namsababishia awe na hasira namfanya kunipiga. Nilinyamaza nikiwa sina hili wala lile kwani sikua na pakwenda.

Jioni moja nilikua nimetoka kanisani, huwa naenda kuimba kwaya kwakua nipo tu nyumbani na mara nyingi nakuwa mpweke, sina sauti ya kihivyo. Nilikua nimeongozana na rafiki zangu wawili, labda niseme waimba kwaya wawili kwani si marafiki kihivyo. “Leo Kaka Iddi hajapost kitu.” Mmoja alilalamika. “Amepost sema naona karudia post, hii nilishaisoma.” Waliongea huku wakionyeshana simu, walikua wanatembea lakini kila mara walikua wakisimama simama.

Nilitamani kuondoka kuwaacha lakini hata sikua na haraka, hakukua na kitu cha maana nilichokua nakiwahi nyumbani, kwanza nilishapika lakini pili wifi yangu alikua nyumbani nayeye ni kisirani kama Kaka yake. Nilisimama nao na kuanza kuangalia walichokua wakikiangalia, niliwaulizaa ndiyo wakaanza kunishangaa kwanini sikufollow. Mmoja alisema huyu hana shida ndoa yake haina matatizo.

Nilimuangalia kwa hasira nikatamani hata kummeza kwani niliona kama ananidhihaki anajua kila kitu katika ndoa yangu. Nilitoa simu yangu na kulike ukurasa wako wa facebook na kisha nikaenda insta nikakufollow. Nilirudi nyumbani na kuanza kukusoma, kwakua nilikua na muda mwingi nadhani ndiyo ilikua kama kazi yangu. Siku tatu baadaye nilinunua Kitabu chako, nilikisoma sana lakini sikuelewa, niliamua kukupigia ndiyo ukaniambia kwa wakati huo nahitaji kujiandaa namna ya kuachika.

Uliniambia maneno ambayo yaliniumiza sana kipindi kile lakini nashukuru uliniambia. Ulisema mume wangu anafahamu anachonifanyia na hata kama nikivumilia vipi ipo siku atachoka kuvumiliwa na ataniacha. Ukaniambia badala ya kuwekeza nguvu zangu katika kunyenyekea na kuhangaika kuwa mke mwema niwekeze nguvu zangu katika kutafuta biashara ya kufanya na kujitegemea mwenyewe.

Nilikuambia kuwa mume wangu hataki nifanye chochote, ukaniuliza kama mimi nilikua nataka atembee na mdogo wangu nilipokuambia hapana uliniambia basi katika maisha si kila mtu anapata kile anachokitaka ni bora mume wangu kuniacha kwakua nafanya kazi kuliko kuniacha kwakua nalialia kila siku kuwa anabadilisha wanawake kama nguo. Wakati ule nakumbuka ulikua bado hujatoa Kitabu chako cha biashara, ulinishauri bure na baada ya kukuambia mazingira yangu uliniambia niuze mchele.

Sikua na mtaji wowote kwani sikua na akiba hata Shilingi kumi, uliniambia hata kama sina mtaji nina vitu ambavyo naweza kuviuza. Ilikua ngumu sana kwangu lakini kitu pekee chenye thamani nilichokua nikimiliki ilikua ni pete yangu ya ndoa. Ilikua na thamani ya kama milioni moja na nusu, niliiuza na kupata milioni moja tu. Mume wangu hata hakua akifuatilia na niliwaza kama akiniuliza basi nimuembie imepotea lakini hakuwahi kuniuliza, isitoshe ilishakua ndogo siivaagi na alikataa kunipa pesa ya kwenda kuirekebisha.

Niliamua kufanya biashara ya mchele kwakua nilikua nafahamiana na mtu yuko mbeya ambaye alikua anafanya hizo biashara na tulipoongea uliniambia kuwa nina marafiki wengi ambao watakua wateja wangu. Niliagiza mzigo lakini kwanza uliniambia kutafuta wateja, nilitafuta nikizungusha sample kidogo na kuchukua oda, kwakua mchana mume yuko bize na mara nyingi harudi nyumbani haikua shida sana mimi kufanya biashara.

Uliniambia nizunguke kwanye migahawa, kwenye Mama lishe na kila sehemu kuulizia oda. Nilifanya hivyo nikaanza biashara, kwakua huyo rafiki yangu alikua mzoefu basia linisaidia, nilianza biashara mwaka jana na mpaka sasa hivi nimeshapata fremu tena sokoni na nina mzigo wa karibu milioni nne. Mume wangu bado hajajua kama nafanya biashara na najua bado anatembea na mdogo wangu, kibaya zaidi nikuwa mdogo wangu ana mimba.

Ingawa sijajua kama ni yakwake au la lakini kwa sasa sitaki kujua, nimemchoka sana mume wangu, ananitia kinyaa, akinigusa nahisi kama ananibaka, nayeye anajua ndiyo maana siku hizi anaishia kunitukana tu hataki tena kufanya mapenzi na mimi. Nina hasira naye mpaka wakati mwingine nawaza hata kumpa sumu kwani ananidharau, ananifanyia ushenzi na wala hajali. Sasa hivi naweza kuondoka, naweza kujitegemea na nikiondoka sirudi kwetu sasa nashindwa niondoke vipi na wanangu kwani siwezi kuondoka na kuwaacha.

***MWISHO
NILIMFUMANIA MUME WANGU NA MDOGO WANGU WA DAMU AKANIPIGA KWA KUMFUMANIA! NILIMFUMANIA MUME WANGU NA MDOGO WANGU WA DAMU AKANIPIGA KWA KUMFUMANIA! Reviewed by Love Psychologist on March 05, 2019 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.